Friday, April 22, 2011

Kikwete abariki nyongeza ya mishahara


ASEMA HATABINAFSISHA TENA TRL, BANDARI
Patricia Kimelemeta

Rais Kikwete akiwa katikati
RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kupitia bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha, 2011/2012. Rais Kikweta alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa akizungumza na viongozi wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mkutano baina ya Tucta na Rais ni wa kwanza tangu Kikwete achaguliwe kwa mara ya pili kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana.

Katika mwaka wake wa mwisho wa ngwe ya kwanza ya uongozi wake, Serikali ya Kikwete iliingia katika malumbano makali kuhusu suala la stahili za wafanyakazi na mishahara midogo iisiyolingana na gharama za maisha.

Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu jana kuwa, pamoja na mambo mengine, Rais ameahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi ili kuwapunguzia makali ya maisha.  “Mishahara ya wafanyakazi ni midogo, ikilinganishwa na kipindi hiki cha kupanda kwa gharama za maisha. Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete ameihaidi kuongeza mishahara kwenye bajeti hii ya fedha ya mwaka 2011/12,”alisema Mgaya.
Mvutano wa Serikali na Tucta
Tukio la Tucta kukutana na Rais Kikwete juzi, linaweza kuwa dalili njema ya kuhitimishwa kwa mvutano baina ya shirikisho hilo na Serikali kuhusu masuala mbalimbali hasa stahili za wafanyakazi.
Mvutano huo uliodumu kwa takriban mwaka mmoja kiasi cha Tucta kutoa tamko kwamba lingewashawishi wafanyakazi kote nchini kutompigia kura mgombea yeyote asiyejali maslahi yao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.

Wakati mvutano huo ukiendelea Mei 4, 2010 Kikwete alilihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuyakataa hadharani mapendelezo ya Tucta ya kutaka kima cha chini cha mshahara cha Sh 350,000/- .
Kikwete alisema hawezi kuwadanganya wafanyakazi kuwa atawaongeza mishahara wanayotaka na yupo tayari kuzikosa kura 350,000 za wafanyakazi.

Baada ya mvutano wa muda mrefu, Agosti 21, 2010 Kikwete akiwa mgombea wa urais kupitia CCM alitamka wakati wa uzinduzi wa kampeni za kitaifa za chama hicho kuwa “mishahara ya wafanyakazi ilikuwa imepanda, ingawa si kwa kiwango kilichokuwa kikitakiwa na Tucta”.
Katika nyongeza hiyo ya mishahara, Serikali ilipandisha kima cha chini kutoka Sh 100,000/- kwa mwezi hadi kufikia Sh235,000/-, tofauti na mapendekezo ya Tucta ya kima cha chini cha Sh315,000/-
Licha ya hatua hiyo, Tucta kupitia kwa Mgaya walibeza kauli hiyo ya Rais wakisema kuwa tangazo hilo lilikuwa limechelewa, huku wakisisitiza
msimamo wao wa kutompa kura mgombea yeyote wa kiti cha urais asiyejali masilahi yao au yule aliyezikataa kura zao.

Reli, Bandari na ATCL Mgaya alieleza pia kuwa katika mkutano huo Rais Kikwete aliahidi kutobinafsisha tena Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), katika kipindi cha uongozi wake.  Kwa mujibu wa Mgaya, Rais ameahidi kampuni hizo sasa kuendeshwa na wazawa ili kuondoa magogoro isiyokuwa na tija kati ya wafanyakazi na waajiri.  Mgaya alisema Rais alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kuondoa migogoro ya wafanyakazi na waajiri wao kama ilivyokuwa ikitokea katika kipindi kilichopita.
"Mbali na hiyo rais amesema, hatua hiyo pia imekusudiwa kuwatumia watalaamu wa ndani ambao pia watasaidia kutetea maslahi ya watumishi wenzao," alisema Mgaya.  “Kuna watalaamu wengi wa kizalendo ambao wamesomeshwa na fedha za walipa kodi lakini, walikosa nafasi ya kuendesha shughuli za mashirika makubwa kama hayo, kutokana na hali hiyo, maamuzi ya Serikali ya sasa ikiwa yatatekelezeka wataweza kuondoa migongano ndani ya maeneo ya kazi," alisema Mgaya.
Mgaya alieleza kuwa Tucta imeamua kuunga mkono hatua hiyo ya Serikali kwa sababu pia inaamini kuwa inaweza kuimarisha mashirika hayo ya umma.  Alisema, katika mkakati huo huo, Rais Kikwete aliwaambia kuwa, Serikali inakusudia kujenga Bandari ya Tanga ili iweze kutoa huduma bora ya usafirishaji katika maeneo hayo na jirani.
  "Rais alisema pia kuwa kutokana na ujenzi huo, Serikali pia itajenga reli yenye hadhi ya kimataifa katika bandari hiyo ili iweze kutoa huduma katika mkoa wa Tanga hadi Arusha na Musoma,"alisema Mgaya akimnukuu Rais Kikwete.  Kwa upande wa Usafiri wa Anga, Serikali inakusudia kutafuta mwekezaji ili aweze kutoa huduma bora za usafiri wa anga nchini, hatua hiyo inafikiwa baada ya Serikali pekee kushindwa kutoa huduma hiyo.  “Kuboresha usafiri wa anga ni gharama, hivyo Serikali  lazima itafute mwekezaji ili aweze kuingia ubia na kutoa huduma hiyo kwa sababu fedha hizo zinaweza kutumika kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya elimu, afya na mengineyo,älisema

No comments:

Post a Comment