Monday, April 25, 2011

Siogopi vitisho, mapambano yapo palepale- Nape

KATIBU wa Halmashuri Kuu, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema atapambana vilivyo kuwang’oa mafisadi waliopo ndani ya chama hicho na kudai katika hilo haogopi mtu na kutotishika na vitisho vinavyoendelea dhidi yake.
Nape alitoa siku 90 kutaka mafisadi kujiondoa wenyewe ndani ya chama hicho na kinyume na hapo watatajwa hadhrani kwani kuwepo kwao wanakiharibu chama hicho na kukiondolea sifa.

Hata hivyo alisema hayo si maamuzi yake binafsi na kudai kuwa ni maazimi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu ya CCM yaliyoazimiwa katika vikao vyake.

Hivyo kufuatia vitisho kwa mafisadi hao amesema katika maisha yake hamwogopi mtu anapotekeleza majukumu yake ya kikazi na kuwataka wafanye wanayoyataka na kusisitiza kuwa amezaliwa katika jiji la Dar es Salaam, hivyo mapambano kwake ni mambo ya kawaida na kamwe hawezi kuogopa watu wanaomtisha.

“Mimi natimiza majukumu yangu nashangaa wanaosema kwamba nafanya mashambulizi yangu kwa ajili ya kuwalenga wanachama fulani”.

“Kwanza mimi namuamini sana Mungu na si kawaida yangu kumuogopa mtu, kwani Mungu akiamua kuniita sitaweza kupinga najua siku yangu ndio imefika’ sitaweza kukwepa” alisema Nnauye

“Sitavunjika moyo, sitakata tamaa na chochote wanachofanya mafisadi ni sawa na kumwagia petroli kwenye moto, matokeo yake ni kuendelea kuulipua na kukoleza mapambano ya vita dhidi yao,”

Hayo yamekuja baada ya kudaiwa kuna baadhi ya wanachama hawataki kujiondoa ndani ya chama hicho na kuleta vikwazo kutokana na hivi karibuni, CCM kuweka mikakati mipya ya kukijenga Chama na kuwataka watuhumiwa wa ufisadi walioko ndani ya CCM kutafakari na kuachia madaraka ndani ya siku 90, vinginevyo watalazimishwa.

Tangu kutangazwa kwa mkakati huo, kuna taarifa kuwa baadhi yao hawataki kuondoka na wamepanga kuanza kutekeleza njama za kuwachafua viongozi waandamizi wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa CCM , Rais Jakaya Kikwete na familia yake.

No comments:

Post a Comment